Kituo cha meli za kitalii chafunguliwa Mombasa

Kenya
Image caption Rais Kenyatta ametangaza kufutiliwa mbali kwa ada ya visa kwa watoto wa chini ya miaka 16 wanaotalii Kenya

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta leo amefungua kituo maalum cha ufukoni cha meli na boti za kitalii kutia nanga mjini Mombasa.

Kituo hicho kwa jina English Point Marina kinatarajiwa kuvutia watalii matajiri wenye kutumia meli na boti za kifahari.

Mkurugenzi wa kituo hicho Alnoor Kanji amesema kituo hicho ni kama "Monte Carlo ndogo" na anatumai kitavutia matajiri wenye kufahia kutalii kwa kutumia meli kama vile Mrusi Roman Abramovich na Bill Gates.

Ndicho kituo cha pekee cha aina hiyo kati ya Cairo, Misri na Cape Town, Afrika Kusini, ambapo majahazi ya kifahari yanaweza kutia nanga na wamiliki wao kupata nafasi ya kujiburudisha.

Image caption Kituo hicho ndicho pekee cha aina yake kati ya Cairo na Cape Town

Ulimwenguni kote maeneo ya Marina huvutia watu walio matajiri zaidi ili kuonyesha mali yao hasa majahazi zao za kifahari.

Ni uwekezaji wa mamilioni ya madola ambao Waziri wa utalii wa Kenya Najib Balala amesema utachangia pakubwa kuimarisha sifa za mji wa Mombasa kitalii.

Kenya imekuwa ikifanya kila juhudi kuwavutia tena maelfu ya watalii walioamua kuiepuka nchi hiyo kutokana na wasiwasi wa kiusalama.

Image caption Bw Kanji amesema kituo hicho ni kama "Monte Carlo ndogo"

Wadau wa Utalii wanasema ufunguzi wa kituo hiki kipya cha English Point Marina ni kifunguo cha mlango mpya wa watalii matajiri ambao kufikia sasa hawakuwa wanavutiwa nchini Kenya na mataifa yenye bandari Afrika Mashariki na Kati.

Ni watalii ambao hupenda safari za majahazi, na huzuru sehemu ambazo wanaweza kutia nanga, huku wakishiriki mashindano ya michezo ya maji au kubarizi.

Matarajio zaidi ni ajira zaidi kwa vijana na washika dau wengine wa sekta mbali mbali hasa kwa sekta ya utalii, ambapo watu takriban 30,000 walipoteza kazi mwaka jana.