Koroma ataka muhula wa tatu Sierra Leone

Ernest Bai Koroma Haki miliki ya picha Getty
Image caption Rais wa Cameroon Ernest Bai Koroma

Wafuasi wa Rais wa Sierra Leone Ernest Bai Koroma wamesema anafaa kuwania urais muhula wa tatu wakisema muhula wa sasa umetatizwa na Ebola.

Wapinzani wake wameonya kwamba hilo litavunja utaratibu wa kikatiba unaoweka kikomo cha mihula miwili ya rais.

Muhula wa sasa wa Rais Koroma unamalizika Februari 2018.

Wafuasi wa Bw Koroma wanasema vita dhidi ya virusi vya ugonjwa wa Ebola, uliowauwa watu wapatao 4,000 katika taifa hilo la magharibi mwa Afrika, vilichukua karibu miaka miwili ya muhula wake wa pili wa utawala, na kwamba anahitaji kubakia madarakani kwa muda zaidi ili akamilishe mipango yake ya kuboresha maisha ya watu wa Sierra Leone.

Lakini makundi ya kiraia yamepinga hatua hiyo, yakisema itasababisha ukiukwaji wa demokrasia nchini humo.

Bwana Koroma alichaguliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2007 na akashinda muhula wa pili na wa mwisho mwaka 2012.

Uchaguzi ujao unatarajiwa kufanyika Februari 2018.

Suala la muhula wa tatu limesababisha mjadala mkubwa barani Afrika, na limezua vurugu nchini Burundi.