Jimenez akamatwa Guatemala

Haki miliki ya picha European Photopress Agency
Image caption Marekani inafanya uchunguzi kuhusiana na ufisadi katika shirikisho la kandanda duniani FIFA.

Polisi nchini Guatemala wamemkamata aliyekuwa rais wa shirikisho la mchezo wa soka nchini humo kama sehemu ya uchunguzi unaoendeshwa na marekani kuhusiana na ufisadi katika shirikisho la kandanda duniani FIFA.

Mshukiwa huyo Brayan Jimenez, amekuwa mafichoni tangu mwezi uliopita wakati Marekani ilipotoa idhini ya kukamatwa kwa maafisa 16, wa shirikisho la soka, katika kanda ya America ya Kusini.

Mshukiwa huyo alikamatwa na polisi katika makaazi ya kibinafsi, katika mji mkuu wa nchi hiyo.

Wakili wake Francisco Garcia Gudiel, amesema sasa atafanya kila juhudi ili mshukiwa huyo asihamishwe hadi Marekani kufunguliwa mashtaka.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Platin na Blatter wote walituliwa kwa miaka minane kutokana na ufisadi katika FIFA

Gudiel amesema yuko tayari pamoja na mawakili wengine kuthibitisha kuwa mshukiwa huyo hana hatia.

Jimenez alikuwa rais wa shirikisho la mchezo wa soka nchini Guatemala Tangu mwaka wa 2010 hadi 2015.

Waendesha mashtaka nchini Marekani wanasema kuwa Jimenez na aliyekuwa katibu mkuu wake jenerali Hector Trujillo, walilipwa hongo ya mamilioni ya madola, ili kuuza haki za utangazaji za mechi za kufuzu za kombe la dunia la mwaka wa 2018.

Trujillo alikamatwa mwezi uliopita nchini Marekani. Kufikia sasa Marekani imewafungulia mashtaka watu 40 kama sehemu ya uchunguzi wake kwenye kashfa ya ufisadi inayokumba FIFA.