Mji wa Addis Ababa hautapanuliwa

Image caption Mji wa Addis Ababa hautapanuliwa

Serikali ya Ethiopia imefutilia mbali mipango yake ya kupanua mipaka ya mji mkuu wa nchi hiyo Addis Ababa, mpango ambao umesababisha vifo na ghasia miezi ya hivi karibuni.

Maandamano yaliyofanywa na watu kutoka jamii ya Oromo, yalichochewa na wasi wasi kuwa wakulima wa jamii hiyo ya Oromo huenda wakatimuliwa kutoka maeneo yao.

Mashirika ya kutetea haki za kibinadam yamekadiria kuwa zaidi ya watu 140 wameuawa na maafisa wa ulinzi wa serikali tangu maandamano hayo kuanza.

Image caption Wakulima wa jamii hiyo ya Oromo walipinga kuondolewa kutoka mashamba yao

Chama tawala katika eneo la Oromia, kimesema kuwa mpango huo umefutiliwa mbali baada ya mazungumzo na wakaazi wa eneo hilo.

Chama cha Oromo People's Democratic Organisation (OPDO) kimechukua uamuzi huo baada ya mazungumzo ya siku tatu.

Chama cha OPDO, kwa ushirikiano na utawala wa Addis Ababa, wangehusika na kutekeleza mradi huo wa upanuzi wa mji mkuu.

Eneo la Oromia ndilo eneo kubwa zaidi nchini Ethiopia na limezingira mji mkuu wa Addis Ababa kutoka maeneo yote.