Islamic State ndio walioshambulia Jakarta

Jakarta Haki miliki ya picha AFP
Image caption Maafisa wa usalama wamezingira eneo hilo

Kundi la Islamic State ndilo lilihusika na mashambulio kadha kwenye mji mkuu wa Indonesia, Jakarta kwa mujibu wa wa shirika la habari lenye uhusiano na Islamic State na polisi wa Indonesia.

Takriban raia wawili na washambuliaji watano waliuawa kwenye shambulio hilo lililotajwa kuwa lililolengwa kufanana na mashambulio yaliyofanyika mjini Paris Novemba mwaka jana.

Vikosi vya usalama vilipambana na washambuliaji kwa saa kadha baada ya wanamgambo hao kulenga biashara kubwa na mitaa yenye biashara nyingi.

Shirika hilo la hahari lenye uhusiano na Islamic State linasema kuwa washambuliaji walilenga watu kutoka mataifa ya kigeni na vikosi vinavyowalinda katika mji wa Jakarta.

Msemaji wa polisi Anton Charliyan alisema kuwa washambuliaji waliiga mashambulio ya Paris.

Alisema kuwa polisi walikuwa wamepokea taarifa mwezi Novemba kuwa Islamic State walikuwa wakipanga “tamasha” nchini Indonesia wakimaanisha shambulizi.

Wawili kati ya washambuliaji hao waliuawa kwenye shambulizi la kujitoa mhanga huku wengine watatu wakiuawa kwenye makabiliano ya risasi na polisi.

Rais wa Indonesia Joko Widodo ameitaka nchi yake isishindwe na vitendo vya kigaidi.

Haki miliki ya picha

Amewahimiza raia wawe na utulivu na kushutumu "kitendo hicho cha ugaidi".

"Tunaomboleza watu waliofariki kwa sababu ya kisa hiki, lakini pia tunakilaani. Kimevuruga utulivu na amani na kuingiza wasiwasi miongoni mwa raia," amesema.

Indonesia, taifa lenye Waislamu wengi zaidi duniani, imeshambuliwa na makundi ya wapiganaji wa Kiislamu awali.

Majuzi, imekuwa kwenye hali ya juu ya tahadhari kutokana na tishio kutoka kwa wapiganaji wa Islamic State.

Hili ndilo shambulio la kwanza kubwa kutokea Jakarta tangu mashambulio kwenye hoteli za Marriot na Ritz mwaka 2009.