Je, Kenya ni taifa la wanyang’anyi?

Mutunga Haki miliki ya picha Willy Mutunga Twitter
Image caption Dkt Mutunga amesema wanasiasa 80% Kenya hawafai kuongoza

Kwa siku kadha sasa mjadala umetawala mitandao ya kijamii Kenya kuhusu matamshi ya Jaji Mkuu Dkt Willy Mutunga kwamba Kenya ni taifa la “wanyang’anyi”.

Dkt Mutunga alisema hayo kwenye mahojiano na gazeti la NRC Handelsblad la Uholanzi.

Kwenye mahojiano hayo, Dkt Mutunga amenukuliwa akisema kwamba wananchi wanapigana vita na magenge ya watu sawa na ‘mafia’ ambayo yanaongozwa na viongozi wa kisiasa na wafanyabiashara wafisadi.

Amesema Kenya ni ngome ya wahalifu wa magenge sawa na makundi ya Al Capone ya miaka ya 1920 nchini Marekani ambayo “yanajizolea mamilioni ya pesa kila siku”.

Anasema ufisadi umekita mizizi kutoka ngazi ya chini ya taifa hadi kileleni.

Dkt Mutunga, kwa mujibu wa gazeti hilo anasema kwa mfano afisa wa polisi anayeitisha hongo kutoka kwa dereva au mwenye gari sharti apeleke sehemu ya hongo hiyo kwa mkuu wake, ambaye vilevile hupeleka sehemu ndogo kwa wakubwa wake. Hili huendelea hivi hadi kufika kwa wakuu wa polisi Nairobi.

“Nguvu za magenge haya ni nyingi. Yanafanya biashara haramu na wanasiasa. Tusipopigana na magenge haya, tunatuwa watumwa wao. Lakini viongozi wanaojitolea kuyakabili ni lazima wawe tayari kuuawa au kwenda uhamishoni,” amenukuliwa.

Je, haya ni kweli?

Kuna baadhi wanaomuunga mkono na kusema amezungumza ukweli mtupu. Mfano ni aliyekuwa mkuu wa tume ya kupambana na ufisadi Prof PLO Lumumba.

"Jaji mkuu ana wadhifa unaomuwezesha kuona mambo ambayo sisi watu wa kawaida hatuwezi kuyaona,” amenukuliwa Prof Lumumba, na kituo cha runinga cha NTV.

"Wale tunaowachagua, wengi wao wameshiriki karamu na shetani mwenyewe.”

Habari hizo zimekuwa zikivuma sana mtandaoni:

Lakini mtazamo huo unapingwa na mwenyekiti wa chama cha Rais Kenyatta cha TNA, Bw Johnson Sakaja, anapinga hayo.

"Unatarajia Waholanzi wafanye nini ukienda kuwaambia jinsi tulivyo wabaya?” anasema na kumlaumu Dkt Mutunga kwa kuenea kwa ufisadi.

Anasema kuna kesi nyingi za ufisadi ambazo zimekwama kwenye mahakama.