Jammeh aondoa marufuku ya nywele Gambia

Jammeh Haki miliki ya picha AFP
Image caption Marufuku hiyo ilikuwa imetolewa mapema mwezi huu

Rais wa Gambia Yahya Jammeh ameondoa agizo la kuwataka wafanyakazi wa kike serikalini wawe wakijifunika nywele wakiwa kazini.

Marufuku hiyo, iliyotolewa tarehe 4 Januari, ilipingwa vikali na makundi ya upinzani.

Imeondolewa kwa sababu imewakasirisha wanawake, afisi yake imesema kupitia taarifa, na kusema kwamba wao (wanawake) ni “marafiki wake wakubwa”.

Afisi ya Bw Jammeh ilisema marufuku hiyo iliyokuwa imetolewa awali “haikuhusiana kwa vyovyote vile na dini” na kwamba wanawake hawafai kukasirishwa nayo.

"Wanawake ni marafiki wakubwa (wa Bw Jammeh), ni dada zake na yuko hapa kwa maslahi na furaha yao kila wakati,” taarifa hiyo imesema.

"Kutokana na hilo, agizo hili ambalo linawakosesha furaha limeondolewa.”

Haki miliki ya picha AFO

Mwezi uliopita, kiongozi huyo alitangaza taifa hilo kuwa Jamhuri ya Kiislamu ingawa aliahidi kwamba watu wa dini nyingine wangeruhusiwa kuendelea na imani zao na hawangelazimishwa kukumbatia mavazi na mitindo ya Waislamu.

Takriban asilimia 90 ya raia wote wa Gambia ni Waislamu.

Bw Jammeh, ambaye ameongoza tangu 1994, hujionyesha kama Mwislamu msalihina na mwenye nguvu za kufanya miujiza.

Aliondoa Gambia kutoka kwa Jumuiya ya Madola 2013 akitaja muungano humo kuwa wa ukoloni mamboleo.

Mwaka 2007, alidai kuwa alikuwa amepata dawa ya kiasili ambayo ingetibu Ukimwi.