Uchunguzi mpya ufanyike Chibok:Buhari

Image caption Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria

Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari ameamuru uchunguzi mpya kufanyika kuhusiana na kutekwa kwa wasichana wa shule ya wasichana ya Chibok kaskazini mwa Nigeria mwaka mmoja na nusu uliopita ambapo zaidi ya wanafunzi 200 walichukuliwa na kundi la wapiganaji la Boko Haram.

Rais Buhari amesema kuwa uchunguzi huo mpya utajikita kubaini mazingira waliotekwa wanafunzi hao na hatua za serikali zilizochukuliwa baada ya utekwaji huo.

Hata hivyo uchunguzi huo wa zaidi ya mwaka na nusu baada ya tukio hauna matumaini kama unaweza kubainisha hasa wapi waliko wasichana hao kutokana na kipindi kirefu kupita.

Tangazo hili la kufanyika kwa uchunguzi mpya kunafuatia mazungumzo kati ya Rais Buhari na wazazi wa watoto hao waliotekwa ambao bado wanashinikiza uchunguzi kuendelea ili kuwapata watoto hao.

Utekaji huo uliofanywa na Boko Haram umekuwa ukilaaniwa Dunia nzima.