Trump asema Cruz hafai kuwa rais Marekani

Cruz Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Trump na Cruz ndio wanaoongoza miongoni mwa wagombea wa Republicann

Mmoja wa wanaopigania tiketi ya kuwania urais kupitia chama cha Republican Donald Trump amemshambulia mgombea mwenzake Ted Cruz kwenye mdahalo akisema hafai kuwa rais wa Marekani.

Bw Trump amesema Seneta Cruz hafai kuruhusiwa kuwa rais nchini Marekani kwa sababu alizaliwa Canada.

Katiba ya Marekani humtaka rais awe mzaliwa wa Marekani.

Bw Cruz amemjibu kwa kumwambia Trump kwamba ameibua suala hilo kwa sababu anapoteza uungwaji mkono katika jimbo la Iowa, wiki mbili tu kabla ya kura za kwanza za kuteua wagombea kupigwa.

Baadaye, aliandika kwenye Twitter kwamba Cruz hafai kuruhusiwa kuwania, akidokeza kwamba akiidhinishwa huenda chama cha Republican kikawasilisha kesi kortini kumpinga.

Wanaopinga msimamo wa Trump wanasema watu waliozaliwa na raia wa Marekani, hata kama wamezaliwa nje ya nchi, huchukuliwa kama raia wazaliwa wa Marekani.

Wanataja mfano wa John McCain ambaye alizaliwa Panama lakini aliruhusiwa kuwania urais.

Trump na Cruz wanaongoza kwenye kura za maoni dhidi ya wagombea wengine watano ambao walishiriki mdahalo huo mjini North Charleston.

Wagombea hao wengine hata hivyo hawakuvuma sana kwenye mdahalo huo.

Masuala ya usalama wa kitaifa, uchumi na sera ya nchi za kigeni pia yalijadiliwa kwenye mdahalo huo.