Burkina Faso:Mateka waokolewa hotelini

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wanajeshi wakikabiliana na wapiganaji katika hoteli ya Splendid

Takriban mateka 30 wameokolewa baada ya wapiganaji kushambulia hoteli moja katika mji mkuu wa Ouagadougou nchini Burkina Faso na kusababisha mauaji ya takriban watu 20.

Watu kadhaa waliofunika nyuso zao walivamia hoteli hiyo ya Splendid,na kuwateka watu kadhaa baada ya bomu kulipuka nje ya hoteli hiyo,kulingana na walioshuhudia.

Waziri wa mawasiliano Remis Danjinou alituma ujumbe katika mtandao wa tweeter akisema takriban wtu 30 wameachiliwa huru na kwamba oparesheni ya kijeshi kukabiliana na wapiganaji hao imeanza.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Upande mmoja wa eneo la mashambulizi ukichomeka

Amesema kuwa waziri wa nguvu kazi Clement Sawadogo ni miongoni mwa waliookolewa.

Tayari takriban watu 30 wamepelekwa hosptalini wakiendelea kupata matibabu aliongezea.

Haijajulikana iwapo kuna mateka ambao bado wamesalia katika hoteli hiyo ,lakini mashahidi wameripoti milio mikali ya risasi katika ghorofa za juu mapema asubuhi.

Image caption Ramani ya eneo lililovamiwa na wapiganaji

Vikosi maalum vya Ufaransa pamoja na wanajeshi wa Burkinabe walihusishwa katika kuwaokoa mateka hao katika hoteli hiyo inayotumiwa na Umoja wa Mataifa pamoja na raia wengine wa Magharibi,alisema bwana Dandinou

Amesema kuwa idadi ya watu waliopoteza maisha yao haijulikani.

Afisa mkuu wa Hospitali Robert Sangare aliwanukuu baadhi ya manusura wakisema takriban watu 20 walifariki katika shambulio la kwanza,kabla ya vikosi vya usalama kuanza makabiliano na wapiganaji hao.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Hoteli ya Splendid Ouagadougou

Baadaye ,waziri wa maswala ya ndani Simon Compaore alisema kuwa miili 10 imepatikana karibu na mgahawa mwengine wa Cappucino ambao pia ulishambuliwa na wapiganaji hao.

Kundi moja linalofuatilia mitandao ya wapiganaji wa Jihad limesema kuwa wapiganaji wa al-Qaeda katika eneo la Maghreb wamekiri kutekeleza shambulizi hilo.