Wanajeshi waliojeruhiwa na al-Shabab wawasili

Image caption Wanajeshi wa Kenya waliojeruhiwa nchini Somali wawsili Kenya

Wanajeshi wa Kenya waliojeruhiwa kwenye shambulio lililofanywa na wapiganaji wa Al-Shabab eneo la el-Ade wamesafirishwa hadi Nairobi.

Wapiganaji hao wa Al-Shabab walishambulia kambi ya jeshi la Umoja wa Mataifa nchini Somalia na kuna ripoti kuwa wanajeshi kadhaa wa Kenya waliuawa huku wengine wakijeruhiwa.

Idadi ya wanajeshi waliouawa haijabainika wazi lakini kundi hilo la Al shabaab linadai kuwa liliwauwa zaidi ya wanajeshi sitini madai ambayo serikali ya Kenya imekanusha.

Image caption Mwanajeshi wa kenya aliyejeruhiwa

Miongoni mwa waliokuwa kwenye uwanja wa ndege wa Wilson kuwalaki wanajeshi hao waliojeruhiwa ni pamoja na waziri wa ulinzi Bi Rachael Omamo na maafisa wengine wa ngazi ya juu jeshini na serikalini.

Omamo amesema habari kuhusu wanajeshi walioangamia zitawasilishwa kwa familia zao moja kwa moja.

Aidha amesema wanajeshi wa Kenya bado wangali wanapambana na wapiganaji hao wa Al shabaab ili kujaribu kuwakomboa wanajeshi waliokwama ikiwa wapo.

Image caption Wanajeshi waliojerihwa

Kenya imekariri kuwa haitaondoa wanajeshi wake Somalia hadi pale kundi hilo la al shabaab litakaposambaratishwa kabisa na amani kurejea nchini humo.

Wakati huo huo kundi hilo limedai kuwa linawashikilia wanajeshi kadhaa wa Kenya mateka.

Al Shabaab limesema ni mara ya kwanza kikosi chake maalum cha Saleh ali saleh Nabhan kilifanya shambulio ndani ya somalia.

Image caption waziri wa Ulinzi nchini Kenya akivihutubia vyombo vya habari

Saleh ali Saleh Nabhan alikuwa kiongozia wa Al qaeda katika kanda ya Afrika mashariki na aliuawa kwenye shambulio lililofanywa na Marekani mwaka wa 2008

Tangu mwaka wa 2011 wakati Kenya ilituma wanajeshi wake nchini Somalia, kundi hilo limefanya mashambulio kadhaa ya kigaidi nchini Kenya na kusababisha maafa makubwa.