Sudan yaombwa kupunguza ada ya mafuta

Image caption Mafuta nchini Sudan Kusini

Taifa la Sudan Kusini huenda likafunga uzalishaji wake wa mafuta katika jimbo la Upper Nile na kufunga mabomba yake hadi pale Sudan itakapokubali kupunguza ada ya usafirishaji wa bidhaa hiyo kulingana na mtandao huru wa Sudan Tribune wenye makao yake nchini Ufaransa.

Mtandao huo umenukuu barua ilioandikwa na wizara ya madini na mafuta nchini Sudan Kusini ikisema:''Hatuna la kufanya ila kufunga kwa sababu haiwezekani.Hatuwezi kuuza mafuta yasio na faida''.

Kwa sasa,Sudan inailipisha Sudan kusini dola 25 kwa kila pipa ili kuruhusu usafirishaji wa bidhaa hiyo kupitia ardhi yake huku bei ya mafuta ikiwa imeshuka hadi kiwango kama hicho cha ada inayotozwa.

Sudan Kusini huzalisha mapipa 160,000 kwa siku.

Ada hiyo ya usafirishaji imekuwa ikizua ugomvi kati ya mataifa hayo mawili tangu Sudan Kusini ijipatie uhuru mwaka 2011.