Zuma akubali Afrika silo bara kubwa zaidi

Zuma Haki miliki ya picha Getty
Image caption Afisi ya Zuma imetoa taarifa wiki tano baada ya Zuma kufanya kosa hilo

Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma ameomba radhi na kusahihisha tamko lake la awali kwamba Afrika ndilo bara kubwa zaidi duniani.

Bw Zuma alitoa matamshi hayo akihutubia dhifa ya jioni ya wafanyabiashara mjini Sandton nchini humo tarehe 9 Desemba mwezi uliopita.

Aliongeza kuwa Afrika ni kubwa kiasi kwamba mabara hayo mengine yanaweza kutoshea ndani ya Afrika.

Alichekwa sana mtandaoni.

Lakini taarifa iliyopakiwa na afisi yake mtandaoni leo inasema: "Afrika bila shaka ndilo bara la pili kwa ukubwa duniani ukizingatia idadi ya watu, na bara kubwa zaidi duniani ni Asia.”

Kwenye taarifa hiyo, afisi hiyo imeonyesha makadirio ya Umoja wa Mataifa kuhusu idadi ya watu mwaka 2015 yanayoonyesha 60% ya watu duniani huishi Asia (4.4 bilioni) na 16% barani Afrika (1.2 bilioni).

Bara Ulaya linafuata kwa kuwa na 10% ya watu (737 milioni).

“Rais amejutia kosa hili.”

Mtandaoni, watu tayari wameanza kuzungumzia taarifa hiyo, baadhi wakisema tayari watu walikuwa wamesahau.

Wengine hata hivyo wanapendekeza Rais Zuma 'arudi shuleni'.

Baadhi nao wamefanyia mzaha taarifa hiyo, kama huyu anayeomba radhi watu wa bara Asia na ulimwengu kwa jumla kutokana na makosa ya kiongozi wake.