Uchumi wa China wapunguza kasi ya ukuaji

Riba Haki miliki ya picha Getty
Image caption Benki kuu ya Uchina imepunguza viwango vya riba mara tatu tangu Novemba 2014

Uchumi wa Uchina ulikua kwa 6.9% mwaka jana, kikiwa kiwango cha chini zaidi cha ukuaji wa uchumi nchini humo katika kipindi cha miaka 25.

Taifa hilo ndilo lenye uchumi wa pili kwa ukubwa duniani.

Ukuaji ulipunguza kasi robo ya nne ya mwaka jana hadi 6.8%. Licha ya tangazo hilo, masoko ya hisa barani Asia hayajaathirika kwani tangazo hilo lilitarajiwa.

Wasiwasi kuhusu hali ya uchumi wa Uchina, pamoja na kupungua kwa mauzo nchi za nje na hata ndani ya nchi vimeathiri sana soko la kimataifa mwaka huu.

Kushuka kwa thamani ya sarafu ya yuan pia kumechangia kuathiri masoko.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Takwimu za hivi majuzi zilionyesha mauzo ya Afrika kwa Uchina pia yalishuka

Takwimu hizi zilizotangazwa kuhusu ukuaji wa uchumi Uchina zinaongeza shinikizo kwa Beijing kuchukua hatua kuimarisha uchumi wake.

Wasiwasi kuhusu ukuaji wa uchumi kumeilazimu benki kuu ya nchi hiyo kupunguza viwango vya riba mara sita tangu Novemba 2014.