Umoja wa Mataifa waiombea Somalia msaada

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Msaada huo utasaidi watu milioni moja nukta moja waliokimbia vita nchini Somalia.

Umoja wa Mataifa na mashirika ya kutoa misaada yametoa wito kwa jamii ya kimataifa kuipa msaada wa takriban dola 885 milioni kuwasaidia zaidi ya watu milioni tano wanaohitaji misaada ya chakula nchini Somalia.

Miongoni mwao wakiwa zaidi ya watoto 310,000 ambao wanakabiliwa na tishio kubwa na kuangamia kutokana na baa la njaa na utapia mlo ikiwa hawatapata misaada ya dharura.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Maelfu ya watu wanakabiliwa na tisho la njaa nchini Somalia

Shughuli za kusambaza misaada zimeathirika pakubwa kutokana na ukosefu wa fedha za kutosha, usalama na mvua ya el nino inayoendelea kushuhudiwa katika sehemu kadhaa.

Mratibu wa umoja wa mataifa anayehusika na masuala ya misaada ya kibinadamu nchini Somalia Peter De Clrecq, amesema wito huo ni muhimu sana na utasaidi watu wengine milioni moja nukta moja waliokimbia vita nchini Somalia.

Miongoni mwa maeneo yaliyoathirika zaidi ni pamoja na Baido, Bossaso, Gaalkayo, Kiismayo na mji mkuu wa Mogadishu.