Ada ya kutumia WhatsApp yaondolewa

WhatsApp Haki miliki ya picha Getty
Image caption Wanaotumia WhatsApp hutakiwa kulipa dola moja baada ya mwaka mmoja

Wamiliki wa app ya mawasiliano ya WhatsApp wamefuta ada ambayo watumizi wake wamekuwa wakitakiwa kulipa kila baada ya mwaka mmoja.

Wamiliki wa huduma hiyo wamekuwa wakiwatoza watu $0.99 kila mwaka baada ya kuitumia kwa mwaka mmoja.

Ada hiyo ilianza kutozwa miaka michache iliyopita lakini kampuni hiyo inasema haijakuwa na manufaa sana.

Taarifa kutoka kwa wamiliki wa WhatsApp inasema: “Watu wengi wanaotumia WhatsApp hawana kadi za benki na wengine huwa na wasiwasi kwamba baada ya mwaka mmoja watazuiwa kuungana tena na marafiki na jamaa.”

“Kwa hivyo, wiki chache zijazo, tutaondoa ada zote tunazotoza wa wanaotumia aina mbalimbali za app yetu na hutatozwa tena pesa ili kutumia WhatsApp.”

Kwa sasa, WhatsApp, ambayo humilikiwa na Facebook, hutumiwa na watu bilioni moja na kampuni hiyo inatumai kuondolewa kwa ada kutavutia watu wengi zaidi.

Haki miliki ya picha Thinkstock
Image caption Kwa sasa WhatsApp hutumiwa na watu zaidi ya bilioni moja

Lakini bado wamesisitiza kwamba hawatakuwa wakiweka matangazo na badala yake watatafuta njia nyingine za kujipatia mapato.