Palin amuunga mkono Donald Trump

Palin Haki miliki ya picha AP
Image caption Palin amesema Trump anaweza kuirejeshea Marekani hadhi

Donald Trump, anayetafuta tiketi ya kuwania urais Marekani kupitia chama cha Republican ameungwa mkono na gavana wa zamani wa Alaska Sarah Palin, aliyewania kiti cha makamu wa rais uchaguzi wa 2008.

"Mko tayari kumuunga mkono Trump?” Bi Palin aliwauliza wafuasi waliokuwa wakimshangilia katika mkutano wa kampeni Iowa.

Alikuwa mgombea mwenza wa John McCain mwaka 2008 waliposhindwa na Barack Obama.

Licha ya kustaafu kutoka kwenye siasa na kujitosa katika bahari ya vyombo vya habari, yeye bado ana wafuasi wengi hasa miongoni mwa wahafidhina.

Akitangaza rasmi kumuunga mkono Bw Trump, Bi Palin amesema mgombea huyo ni mtu ambaye yuko tayari kuwawezesha wanajeshi wa Marekani kuangamiza kundi linalojiita Islamic State.

"Tuko tayari kwa mabadiliko,” amesema katika mkutano huo mjini Ames, Iowa.

"Yeye anatumikia “sisi raia”, hatumikii mtu mwingine. Yuko kwenye nafasi nzuri sana ya kuirejeshea Marekani hadhi yake tena.”

Bw Trump baadaye kupitia taarifa amesema anajivunia kuungwa mkono na Bi Palin.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Bw McCain na Bi Palin mwaka 2008

Bi Palin alikuwa amehudumu kama gavana wa Alaska miaka miwili alipoteuliwa na John McCain kuwa mgombea mwenza wake.

Alikuwa akivutia umati mkubwa wa watu mikutanoni na kuangaziwa sana na vyombo vya habari.

Baada ya uchaguzi mwaka 2009, alijiuzulu wadhifa wa ugavana na akaanza kufanya kazi kama mwandishi wa habari na mdadisi wa masuala ya kisiasa.

Kabla ya kutangaza kumuunga mkono Bw Trump, Bi Palin alikuwa amesambaza makala ya mtandaoni iliyoandikwa na bintiye Bristol ambayo inamshambulia mpinzani mkubwa wa Trump katika jimbo muhimu la Iowa, Ted Cruz.

Jimbo hilo ndilo litakalokuwa la kwanza kupiga kura za kuamua mgombea.

Bw Cruz hata hivyo amemsifu Bi Palin akisema "bila uungwaji mkono wake, singekuwa katika bunge la seneti”, akirejelea uungwaji mkono aliopata wakati wa duru ya pili ya uchaguzi wa useneta mwaka 2012.

"Bila kujali atakayofanya 2016, nitabaki kuwa mfuasi wake mkuu,” ameandika kwenye Twitter.