Watu wenye silaha wavamia chuo kikuu Pakistan

Watu wenye silaha wameshambulia chuo kikuu kimoja eneo la Charsadda kaskazini magharibi mwa Pakistan.

Washambuliaji walijaribu kuingia ndani ya chuo kikuu cha Bacha Khan kwa nguvu na makabiliano kati yao na maafisa wa usalama bado yanaendelea, ripoti zinasema.

Milipuko miwili mikubwa imesikika, afisa wa polisi ameambia shirika la habari la Reuters.

Ripoti zinasema watu wawili wamejeruhiwa. Maafisa wa usalama wamezingira chuo kikuu hicho.

Eneo la Charsadda liko umbali wa kilomita 50 (maili 30) kutoka jiji la Peshawar, ambako wapiganaji wa Taliban waliua zaidi ya wanafunzi 130 baada ya kushambulia shule moja.