Jamie Foxx aokoa dereva

Oscars Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Foxx ni mmoja wa waigizaji weusi waliowahi kushinda tuzo za Oscars

Mwigizaji mashuhuri Jamie Foxx alimuokoa mwanamume kutoka kwa gari lililokuwa linaungua moto baada ya ajali kutokea karibu na nyumba yake California.

Ajali hiyo ilitokea Jumatatu jioni baada ya gari hilo kugonga bomba la maji.

Foxx anasema alisikia kishindo na kupigia simu maafisa wa huduma za dharura na kisha akatoka nje ambapo alimpata dereva amekwama ndani ya gari hilo.

Afisa wa huduma za dharura alifika haraka na kwa pamoja wakasaidiana kumtoa dereva huyo aliyetambuliwa kama Brett Kyle, 32, kutoka kwenye gari.

Haki miliki ya picha EVN
Image caption Gari hilo lilishika moto sekunde tano baada ya Kyle kutolewa

Gari hilo lilishika moto “sekunde tano tu” baada yao kumtoa dereva huyo kutoka garini, Jamie baadaye alieleza.

Mwigizaji huyo aliyewahi kushinda tuzo ya Oscar ameambia kituo cha habari cha CBS Los Angeles, kwamba: "Sitazami tukio hili kama tukio la kishujaa.

“Naliona tu lilivyo, unajua, ilikuwa ni lazima ningefanya kitu. Na kwa bahati nilifanikiwa.”

Kyle alipata majeraha na anaendelea kupata nafuu.