Magufuli amsimamisha kazi mkuu wa uhamiaji

Magufuli Haki miliki ya picha Statehouse Tanzania
Image caption Idara ya uhamiaji imekabiliwa na tuhuma za rushwa na utendaji mbovu

Rais wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli amemsimamisha kazi Kamishna Mkuu wa Uhamiaji nchini humo Sylvester Ambokile kupisha uchunguzi katika idara ya uhamiaji.

Taarifa kutoka kwa kaimu mkurugenzi wa mawasiliano ya ikulu Gerson Msigwa imesema Bw Ambokile amesimamishwa kazi kutokana na tuhuma za rushwa, ukusanyaji mbaya wa maduhuli ya serikali, ukiukwaji wa taratibu za manunuzi na utendaji mbovu.

Tuhuma hizo zilibainika wakati waziri wa mambo ya ndani ya nchi Bw Charles Kitwanga alipotembelea idara ya uhamiaji hivi karibuni

Kamishna wa Uhamiaji anayeshughulikia Utawala na fedha Bw Piniel Mgonja pia amesimamishwa kazi.

Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue amesema watendaji hao wakuu wa uhamiaji wamesimamishwa kazi mara moja hadi hapo uchunguzi utakapokamilika.

“Endapo watabainika kutokuwa na makosa Rais ataamua hatima yao,” amesema.

Hayo yakijiri, Dkt Magufuli pia amemrejesha Bw Eliakim Chacha Maswi kuwa katibu tawala wa mkoa wa Manyara, baada ya kuhudumu kipindi kifupi katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Bw Maswi alikuwa ameteuliwa kuwa kaimu naibu kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)

“Rais Magufuli amefanya mabadiliko hayo kwa lengo la kumtafuta mtu mwenye utaalamu wa kuendeleza kazi iliyofanywa na Bw Maswi,” Bw Sefue amenukuliwa katika taarifa hiyo kutoka ikulu.

Tangu kuchukua madaraka mwezi Novemba mwaka jana, Dkt Magufuli amewasimamisha au kuwafuta kazi maafisa wengi wakuu serikalini.