Seif Idd: Zanzibar yasubiri uchaguzi

Matokeo
Image caption Matokeo ya uchaguzi Zanzibar yalifutwa na tume ya uchaguzi

Makamu wa pili wa serikali ya Zanzibar Bw Seif Ali Idd amesema wakazi wa Zanzibar wanasubiri kutangaziwa tarehe ya kufanyika kwa uchaguzi.

Aidha Bw Idd amesema kuwa hali Zanzibar ni shwari na hakuna sababu ya kuwa na wasiwasi.

Alisema hayo alipokutana na Rais wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli katika ikulu jijini Dar es Salaam.

"Mimi nimekuja kumpa taarifa juu ya hali yetu Zanzibar inavyokwenda, nimemueleza kwamba Zanzibar ipo salama, Zanzibar ina utulivu na ina amani," amesema Bw Idd, kwa mujibu wa taarifa kutoka ikulu.

Haki miliki ya picha Statehouse Tanzania
Image caption Seif Idd alikutana na Rais Magufuli ikuluni Dar es Salaam

"Hayo yanayoandikwa kwenye magazeti kuwa Zanzibar kuna fujo, Zanzibar kutatokea machafuko sio kweli, na kama unavyojua uchaguzi ulifutwa na tume ya uchaguzi na tunasubiri tarehe mpya ya uchaguzi itangazwe na tume ili tufanye uchaguzi.”

Wazo la kurudiwa kwa uchaguzi visiwani limepingwa vikali na Chama cha Wananchi (CUF) ambacho badala yake kinataka mshindi wa uchaguzi uliofanyika 25 Oktoba mwaka jana atangazwe.

Viongozi wa chama hicho walisusia maadhimisho ya Siku ya Mapinduzi Jumanne wiki iliyopita, sherehe ambazo zilihudhuriwa na Dkt Magufuli na viongozi wengine wa Tanzania.