Zana za kijeshi zaibiwa Burkina Faso

Image caption Hali ilivyokuwa nje ya ghala la silaha la Yamdi mapema leo

Kikosi cha kumlinda rais kilichovunjwa nchini Burkina Faso kimeendesha uvamizi usiku katika ghala la silaha la serikali karibu na mji mkuu, kwa mujibu wa msemaji wa jeshi.

Kanali Williame Yameogo alisema kuwa hakukuwa na visa vya majeruhi wakati wa uvamizi huo ambao ulifanyika mwendo wa saa tisa usiku saa za nchi hiyo katika ghala la silaha la Yamdi.

Habari zingine za kijeshi zilisema kuwa watu wenye silaha waliwazidi nguvu walinzi kabla ya kutoroka na kiwango cha silaha kisichojulikana

Kikosi cha kumlinda rais kilihusika kwenye mapinduzi ya kijeshi yaliyodumu kwa muda mfupi mwezi Septemba.

Kiongozi wa mapinduzi hayo Gilbert Diendere ambaye alikuwa mshirika wa karibu wa aliyekuwa rais Blaise Compaore akisubiri kuhukumiwa.

Bwana Compaore alipundiliwa wakati wa mapinduzi ya mwaka 2014 baada ya kuwa madarakani kwa miaka 27.