Pesa ziko wapi duniani?

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Viongozi mashuhuri duniani wanakutana Davos, Uswizi kujadili uchumi wa dunia

Viongozi mashuhuri duniani wanakutana mjini Davos kujadili uchumi wa dunia. Moja ya masuala watakayojadili ni usawa katika kumiliki mali, jambo ambalo wengi wanaamini ni tatizo linalozidi kuongezeka.

Credit Suisse, benki moja ya Uswizi, huchapicha ripoti kila mwaka kuhusu utajiri duniani, ikiangazia maeneo ambayo utajiri upo duniani kwa kuangalia taifa na kanda pia.

Hali iko vipi ukilinganisha maeneo tajiri duniani na maeneo maskini, na je kuna mabadiliko?

Hii hapa ni ramani ya kuenea kwa utajiri duniani 2015, kwa mujibu wa Credit Suisse.

Utajiri Amerika Kaskazini

Sehemu kubwa ya utajiri duniani umo Marekani, Canada na Ulaya.

Credit Suisse inasema kiasi cha kadiri cha utajiri wa mtu mzima Amerika Kaskazini, ukiondoa Mexico ambayo imewekwa kundi moja na nchi za Amerika Kusini, ni US$342,000.

Utajiri hapa una maana ya thamani ya bidhaa zote, pesa na mali, ukiondoa madeni.

Kiwango cha utajiri katika maeneo hayo ni cha juu mno ukilinganisha na maeneo mengine duniani. Ni karibu mara 75 zaidi ya kiwango cha kadiri cha utajiri Afrika na India, na zaidi ya mara 15 kiwango cha utajiri Uchina na Amerika Kusini.

Aidha, ni mara 2.5 zaidi ya kiwango cha kadiri cha utajiri Ulaya.

Kumbuka ripoti hii inatumia dola kwenye hesabu zake, na haizingatii tofauti katika uwezo wa kununua bidhaa, hivyo basi hakuna njia ya kubaini athari ya gharama ya juu ya maisha kwenye utajiri wa mtu.

Huenda ukawa na dola nyingi Marekani lakini pesa hizo zisikuwezeshe kununua kiasi sawa cha bidhaa au kulipia huduma sawa katika taifa jingine.

Kwa sababu mali ni sehemu kubwa ya utajiri, thamani ya mashamba na ardhi katika baadhi ya kanda huenda pia ikachangia tofauti kubwa inayoonekana.

Takwimu hizi zinatumia kiwango cha kadiri cha utajiri (jumla ya utajiri unagawa na idadi ya watu wazima) badala ya kiwango cha kati cha utajiri, kiasi cha utajiri ambao watu wengi wanao katika taifa fulani.

Hii ina maana kwamba kukiwa na watu matajiri wa kupindukia, kiasi cha wastani cha utajiri katika taifa fulani kinaweza kikawa juu sana kuliko cha raia wengi.

Watu asilimia 1 matajiri kupindukia huishi wapi?

Ripoti hiyo inaangalia ni wapi watu 1% matajiri zaidi duniani wanapatikana.

Mataifa kumi yanayochangia watu 1% matajiri wa kupindukia duniani:

  1. Marekani 20,680,000 (wameongezeka 15% ukilinganisha na 2014)
  2. Uingereza 3,623,000 (wameongezeka karibu 25%)
  3. Japan 3,417,000 (wameshuka kwa zaidi ya 15%)
  4. Ufaransa 2,762,000 (wameshuka kwa karibu 22%)
  5. Ujerumani 2,281,000 (wameshuka kwa zaidi ya 17%)
  6. Uchina 1,885,000 (wameongezeka kwa zaidi ya 19%)
  7. Italia 1,714,000 (wameshuka kwa karibu 25%)
  8. Canada 1,500,000 (wameshuka kwa zaidi ya 7%)
  9. Australia 1,480,000 (wameshuka kwa 17%)
  10. Uswizi 831,000 (wameongezeka kwa zaidi ya 3%)

Takwimu zinaonyesha idadi ya matajiri wa kupindukia inaongezeka Uchina (wameongezeka kwa 19%), Amerika Kaskazini (wameongezeka kwa 20%) na UIngereza (wameongezeka kwa karibu 25%), na inashuka kwingineko, hasa katika mataifa mengi tajiri Ulaya, Japan na Australia.

Hii inaweza kuwa na maana kwamba uchumi wa Uchina unazalisha mamilionea wengi, au kwamba matajiri wa kupindukia wanatumia fursa ya kuhamisha mali kwa urahisi kuhamia vitovu vya kibiashara, kama vile London au New York.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Matajiri wanaonekana kuongezeka Uchina

Lakini kubadilika sana kwa thamani sekta ya ardhi na nyumba huenda pia kukaathiri sana matajiri.

Iwapo unamiliki nyumba London bila mkopo, kwa mfano, bila shaka wewe ni kama “tajiri wa kupindukia”, ukifuata vigezo vya Credit Suisse.