UK na Gates watoa pesa za kukabili Malaria

Mpango Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mpango huo utadumu kwa miaka mitano

Serikali ya Uingereza na bwanyenye Bill Gates wametangaza mpango wa dola bilioni nne wa kusaidia kukabiliana na ugonjwa wa Malaria.

Mradi huo utahusisha ufadhili kwa utafiti wa kutafuta dawa mpya za kutibu Malaria pamoja na dawa za kuua mbu.

Pesa hizo zitajumuisha £500 milioni kila mwaka kutoka kwa mfuko wa misaada wa Uingereza kwa nchi za nje kwa kipindi cha miaka mitano, pamoja na $200 milioni kutoka kwa Wakfu wa Gates.

Bill Gates na Waziri wa fedha wa Uingereza Geroge Osborne, kwenye makala ya pamoja kwenye jarida la The Times, wameeleza matumaini kwamba Malaria itaangamizwa.

Maradhi hayo huua mtoto mmoja kila dakika, wengi wakiwa barani Afrika.

Malaria imetajwa kuchangiwa zaidi na hali ya umaskini.

Juhudi za kukabiliana na ugonjwa huo zimepiga hatua katika kipindi cha miaka 15 iliyopita, lakini kuna tishio la kuenea kwa viini vya malaria visivyosikia dawa pamoja na mbu wasiosikia dawa, WHO ilisema kwenye ripoti yake kuhusu Malaria duniani ya 2015.

"Iwapo dawa mpya hazitatengenezwa kufikia 2020, hali huenda ikawa mbaya na vifo kuongezeka,” Bw Osborne na Bw Gates wamesema.

Ufadhili huo umetangazwa siku chache tu baada ya Bw Gates kutangaza atatoa $100 za kusaidia kukabiliana na utapiamlo nchini Nigeria.