Buhari kuhudhuria ibada ya wanajeshi Kenya

Buhari Haki miliki ya picha AFP
Image caption Buhari atakuwa nchini Kenya kwa ziara rasmi ya siku tatu

Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari ataungana na Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta kwenye ibada ya maombi ya kuwakumbuka wanajeshi wa Kenya waliouawa Somalia.

Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamoud pia atahudhuria ibada hiyo.

Kiongozi huyo wa Nigeria atawasili Kenya Jumatano kwa ziara rasmi ya siku tatu na kwenda moja kwa moja kuhudhuria ibada hiyo.

Kinyume na ilivyo kawaida, ambapo viongozi wengi mashuhuri hulakiwa Nairobi, Bw Buhari atalakiwa na mwenyeji wake Bw Kenyatta katika uwanja wa kimataifa wa ndege wa Eldoret, ulioko Magharibi mwa Nairobi.

Ibada ya maombi itafanyika katika kambi ya jeshi ya 9th Kenya Rifles, Moi Barracks, viungani mwa mji huo wa Eldoret.

Wengi wa wanajeshi waliouawa baada ya wapiganaji wa al-Shabab kuvamia kambi ya el-Adde, kusini magharibi mwa Somalia tarehe 15 Januari walitoka kambi hiyo.

Wapiganaji wa al-Shabab wamesema waliwaua wanajeshi zaidi ya 100 wa Kenya kwenye shambulio hilo, habari ambazo serikali ya Kenya imekanusha.

Kenya na Nigeria zimekuwa zikiimarisha uhusiano.

Septemba 2013, aliyekuwa Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan alizuru Kenya na hata akahutubia kikao cha pamoja cha mabunge yote mawili.

Mei 2014, Rais Kenyatta alifanya ziara rasmi Nigeria.