Shirika la Planned Parenthood laondolewa makosa

CMP Haki miliki ya picha Getty
Image caption Shirika la CMP limekuwa likipinga shughuli za Planned Parenthood

Wanaharakati wa vuguvugu la kukabiliana na utoaji mimba walinasa kwa siri kanda ya video kama hatua ya kushinikiza kusitishwa ufadhili kwa shirika la Planned Parenthood linalohusika na afya ya uzazi.

Planned Parenthood ni shirika lisilo la serikali na hutoa huduma za afya ya uzazi kwa raia wa kipato cha chini nchini Marekani.

Baadhi ya vituo vyake hutoa huduma za kuavya mimba.

Maafisa wa vuguvugu hilo la Center for Medical Progress (CMP) wanadaiwa kujifanya wanunuzi wa viungo vya vijusi na kunakili kikao chao na maafisa wa Planned Parenthood kwenye video.

Video hiyo ilihaririwa kabla ya kutolewa, lengo kuu likiwa kushinikiza shirika hilo la afya ya uzazi linyimwe ufadhili.

Shirika hilo limelalamika kwamba kanda hiyo ilihaririwa na haikua ukweli wa mambo. Planned Parenthood imekiri kutoza ada za chini kwa wale wanaotaka vijusi na kwamba fedha siyo faida kwake.

Mwanzilishi wa CMP David Daleiden ameshtakiwa makosa ya kununua viungo vya binadamu.

Wanachama wa Republican pamoja na bunge la Congress walijadili kuhusu kanda hiyo na kutaka serikali kuu kusitisha ufadhili wake kwa Planned Parenthood.

Upande wa Democtrats wamesalia kimya na Rais Obama ameahidi kupinga mswada wa kusitisha ufadhili kwa shirika hilo.

Majimbo, 11 pamoja na Texas yameanza uchunguzi dhidi ya kanda hiyo.