Wapinga sheria ya uavyaji mimba S Leone

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Ernest bai Koroma

Viongozi wa kikristo na wenzao wa kiislamu wametoa wito kwa raia kujiunga nao katika maandamano hadi bunge wakitaka kuondolewa kwa sheria tata ya uavyaji mimba.

Sheria hiyo inaruhusu mimba za hadi wiki 12 kutolewa bila sababu.

Huo ndio utata unaozunguka sheria hiyo huku viongozi wa dini wakisema kuwa ''ni sawa na mauaji''.

Wanaounga mswada huo wanasema kuwa utasaidia kumaliza uavyaji mimba wa mitaani ambao husababisha vifo miongoni mwa wanawake wajawazito.

Sheria hiyo pia inasema kuwa mimba kutoka wiki 13 hadi 24 zinaweza kutolewa iwapo zinatishia maisha ya mama, kuna tatizo katika mtoto ama iwapo mimba hiyo ilisababishwa na ubakaji au ndugu.

Bunge lilipitisha mswada kwa umoja mnamo mwezi Disemba,lakini rais alikataa kuutia saini baada ya viongozi wa dini kuwasilisha malalamishi yao.

Rais huyo amelirudisha pendekezo hilo bungeni, na viongozi wa dini wanatumai kwamba maandamano hayo yatashinikiza kuondoa sheria hiyo.