Al-Shabab waingia na kudhibiti el-Adde

Al-Shabab Haki miliki ya picha AP
Image caption Majeshi ya Kenya yamekuwa yakikabiliana na al-Shabab nchini Somalia tangu 2011

Wapiganaji wa al-Shabab wameingia na kudhibiti miji ambayo majeshi ya Kenya yaliondoka jana nchini Somalia.

Wakazi wameambia BBC kwamba wapiganaji wa kundi hilo la Kiislamu wamesema wapiganaji hao wameingia kwenye miji ya Al-Adde, Hosingoh na Badhaadhe.

Katika mji wa Hosingoh, mamia ya wapiganaji wanaripotiwa kuingia na kuhutubia wakazi na kisha wakamteua kiongozi wa kusimamia eneo hilo.

Majeshi ya Kenya yaliondoka miji hiyo siku chache baada ya kambi yao el-Adde kushambuliwa.

Kundi hilo lilisema liliwaua wanajeshi 100, lakini habari hizo zimepuuziliwa mbali na serikali ya Kenya.

Serikali ya Kenya, hata hivyo, bado haijatoa idadi ya wanajeshi wake waliouawa au kujeruhiwa wakati wa shambulio hilo la tarehe 15 Januari.

Akizungumzia kuondoka kwa majeshi ya Kenya maeneo hayo ya kusini mwa Somalia, msemaji wa majeshi ya Kenya Kanali David Obonyo alisema ni jambo la kawaida.

Kanali Obonyo amesema kuondoka kwa wanajeshi hao ni moja moja tu ya mipango ya kijeshi na hakufai kutazamwa kama kuondoka kabisa kwa wanajeshi eneo hilo.

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta leo aliungana na Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari na Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamoud kwa ibada ya kuwakumbuka wanajeshi waliouawa.

Ibada hiyo ilifanyika katika mji wa Eldoret, magharibi mwa Kenya.

Kenya ina wanajeshi takriban 4,000 nchini Somalia ambao huhudumu chini ya majeshi ya kulinda amani ya Muungano wa Afrika (Amisom).