Gbagbo akanusha mashtaka ya uhalifu ICC

Gbagbo Haki miliki ya picha AP
Image caption Gbagbo akiingia mahakamani ICC

Rais wa zamani wa Ivory Coast Laurent Gbagbo na kiongozi wa vijana waliomuunga mkono Charles Ble Goude wamefika mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai mjini The Hague nchini Uholanzi.

Wanakabiliwa na mashataka ya madai ya kuhusika kwao kwenye vurugu za baada ya uchaguzi mkuu nchini Ivory Coast mwaka wa 2011.

Gbagbo amekanusha mashtaka manne ya uhalifu dhidi ya binadamu baada ya kusomewa mashtaka hayo ICC.

Bw Gbagbo na mwenzake, kiongozi wa vijana waliomuunga mkono Bw Gbagbo, Bw Ble Goude, wote wawili wamekanusha mashtaka ya kuandaa “mpango wa pamoja” ambao ulisababisha mauaji, ubakaji, kuteswa kwa raia na “matendo mengine ya kinyama”, mwandishi wa BBC aliyeko The Hague Anna Holligan anasema.

Awali, kumezuka mtafaruku baada ya wafuasi takriban 50 wa kiongozi huyo wa zamani, waliokuwa wakiimba na kupeperusha bendera, kukabiliana na maafisa wa usalama nje ya majengo ya mahakama.

Kesi hiyo imesubiriwa kwa takriban miaka mitatu ama minne hivi.

Bw Gbagbo awali alikuwa amewasilisha ombi la kutaka aachiliwe huru kwa misingi ya kiafya. Ombi lake lilikataliwa mwezi Septemba mwaka jana.

Wote wawili wanatuhumiwa kwa makosa manne ya uhalifu, mauaji, ubakaji, vitendo vya kinyama na mateso kwa binaadamu madai ambayo wote wawili wameyakana.

Mahakama hiyo ya ICC inaangalia zaidi ushahidi utakaotolewa wa waathiriwa wa matendo ya wawili hao pindi walipokuwa mamlakani na inatarajiwa mwakilishi wao atafika mahakamani kupata maamuzi ya mahakama mjini The Hague.

Mwendesha mashtaka wa mahakama hiyo ya ICC, Fatou Bensouda anatarajiwa kuwasilisha ushahidi wa kuthibitisha kuwa machafuko ya mwaka 2011, kufuatia Laurent Gbagbo kukataa ushindi wa mpinzani wake Alassane Ouattara, yalikuwa sehemu ya mpango ulioandaliwa, na ulioungwa mkono na majeshi yake na hivyo kumuwezesha Gbagbo kusalia madarakani.

Miezi mitano baada ya uchaguzi, ghasia zilizuka na watu wapatao 3000 wakapoteza maisha.

Lakini wakili wa Laurent Gbagbo, anadai kwamba rais huyo wa zamani wa Ivory Coast alipokonywa ushindi wake na Umoja wa Mataifa na kuingiliwa na nchi ya Ufaransa, na kusababisha kukamatwa kwake Aprili mwaka huo wa 2011.

Kesi hii inaweza kuwa muhimu kwa mustakabali wa baadaye wa mahakama ya ICC. Ambayo imekuwa ikikabiliwa na upinzani katika miaka ya hivi karibuni, ikiwa ni pamoja na kutoka kwa wakuu wa sasa wa mataifa ya Afrika, kwa madai kuwa mahakama hiyo inawalenga watu weusi pekee.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Wafuasi wa Bw Gbagbo wamefika na kukusanyika nje ya mahakama

Mnamo mwezi Desemba mwaka 2015, ilalizimika kufuta madai yaliyokuwa yakimkabili Rais wa Kenyan Uhuru Kenyatta, kwa kutokuwa na ushahidi wa kutosha dhidi yake. Na kufuatia suala hilo, inadaiwa kwamba hadhi ya mahakama hiyo imeshuka.

Kesi hii itaamua mustakabali wa Laurent Gbagbo na Charles Ble Goude. Lakini wengi wanasema ni muhimu pia kwa Mahakama hiyo kuweza kuthibitisha uadilifu wake kwa ulimwengu, na uaminifu wake upande wa mashtaka ili kuhakikisha mustakabali wa ICC yenyewe.

Bw Gbagbo ndiye rais wa kwanza kushtakiwa na mahakam ya ICC.