Nani mfisadi zaidi Kenya?

Mutunga Haki miliki ya picha Willy Mutunga Twitter
Image caption Majuzi, Jaji Mkuu Mutunga alisema Kenya imeshikwa mateka na 'magenge ya wanyang'anyi'

Nani mfisadi zaidi Kenya? Ndilo swali ambalo limejitokeza baada ya viongozi wawili wakuu wa Bunge na Mahakama kujibizana mtandaoni.

Chanzo cha majibizano haya ni taarifa ambayo Jaji Mkuu Dkt Willy Mutunga aliitoa akitangaza kwamba alikuwa amepotea habari za madai ya ufisadi dhidi ya jaji mmoja wa Mahakama ya Juu.

Jaji huyo anatuhumiwa kupokea hongo ya $2 milioni ili kupendelea upande mmoja kwenye kesi ya uchaguzi.

Dkt Mutunga alisema uchunguzi ulifanywa na kikao maalum cha Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) kingeandaliwa Jumatano kujadili matokeo ya uchunguzi huo.

Kiongozi wa Wengi Bungeni, Bw Aden Duale, ambaye ndiye anayewakilisha serikali Bungeni, akichangia kwenye taarifa hiyo aliandika: “Sasa Jaji Mkuu amethibitisha kwamba idara ya mahakama na mahakama ya juu hasa, imejaa ufisadi.”

Akimjibu, Jaji Mutunga alisema: “Ninaweza kuthibitisha kwamba idara ya mahakama haitawahi kufikia viwango vya ufisadi ambavyo vimefikiwa na Bunge.”

Majuzi, Dkt Mutunga alisema Kenya ni taifa ambalo limeshikwa mateka na wanyang’anyi na kwamba ufisadi umesheheni katika kila ngazi ya uongozi.

Alinukuliwa na gazeti moja la Uholanzi akisema magenge hayo ya watu, ambayo ni sawa na ‘mafia’, yanaongozwa na viongozi wa kisiasa na wafanyabiashara wafisadi.