Mvutano kuhusu WhatsApp Afrika Kusini

Image caption Mvutano kuhusu WhatsApp Afrika Kusini

Kampuni kubwa za kutoa huduma za mawasiliano nchini Afrika Kusini zimeitaka tume inayoisimamia mawasiliano ya nchi hiyo kudhibiti matumizi ya programu za mawasiliano ya mitandao ya kijamii kama vile WhatsApp na Skype

Maafisa wakuu wa kampuni ya MTN na Vodacom walifika mbele ya kamati ya bunge la Afrika Kusini wakitaka huduma ya bei nafuu ya intaneti inayotambuliwa kama over-the-top (OTT) internet , idhibitiwe.

Kauli yao hata hivyo ilipingwa na kampuni ya Cell C inayodai kuwa makampuni hayo makubwa yanalenga kukandamiza mawasiliano na ubunifu.

MTN na Vodacom zinatoa hoja kuwa huduma ya mitandao hiyo ya OTT zinatumia mitandao yao pasi na malipo kamili kwani kwa sasa mtu anaweza kutumia programu hizo WhatsApp na Skype kupiga simu.

Kamati hiyo ya bunge inayosimamia mawasiliano na huduma za posta inatafuta ukweli kuhusu mbinu za kuweka sheria za kuthibiti vyombo vya mawasiliano na huduma za OTT.