Wasomali waandamana dhidi ya Al-shabaab

Image caption Raia wa Somalia wakiandamana dhidi ya shambulio la mgahawa wa Lido Beach Resort

Kundi la raia wa Somalia limefanya maandamano ya amani katika eneo la shambulio la kigaidi lililofanyika wiki iliopita katika mji mkuu wa Mogadishu.

Wapiganaji kutoka alshabaab waliwaua watu 20 wakati walipolenga ufukwe wa bahari wa hoteli ya Lido Beach Resort.

Waandamanaji hao ambao waliwaunga mkono waathiriwa,walilishtumu kundi hilo wakisema 'halina dini'.

Umaarufu wa hoteli ya Lido Beach umeonekana ishara ya kurudi kwa hali ya kawaida mjini Mogadishu baada ya miaka mitatu ya mgogoro.

Ufukwe huo huwavutia maelfu ya vijana wa Kisomali ambao hujiliwaza na kufurahia mazingira yake pamoja na mchezo wa kuruka mawimbi.

Alshabaab imesema kuwa ililenga mgahawa huo kwa sababu hutembelewa sana na maafisa wa serikali.

Image caption Maafisa wa serikali walitumia neno Ugus wakimaanisha shirika linalowaua raia bila hatia

Msemaji wa mamlaka ya mji wa Mogadishu ,ambayo ilipanga mkutano huo,iliambia BBC Somali kwamba walikutana ili kupinga vitendo vya kundi hilo.

''Walitaka kuonyesha kutoridhishwa kwao na kile kilichotokea hapa,ambacho ni kisa cha mauaji wa raia wasio na hatia,''Abdifitah Omar Halane alisema.

Kundi la Alshabaab ambalo ni kitengo cha Al Qaeda,liliondolewa mjini Mogadishu mnamo mwezi Agosti 2011,lakini bado linadhibiti maeneo mengi ya kusini mwa Somalia.