Viongozi wa Afrika wakutana kujadili Burundi

Huwezi kusikiliza tena

Viongozi wa mataifa ya Afrika wameanza kuwasili mjini Addis Ababa kwa mkutano mkuu wa Muungano wa Afrika ambao unatarajiwa kujadili hali nchini Burundi.

Vongozi hao kadhalika watajadili mgogoro wa kisiasa nchini Sudan Kusini.

Kwa sasa, mawaziri kutoka nchi wanachama wa AU wamekuwa wakikutana kuandaa mapendekezo ambayo yatakabidhiwa kwa viongozi hao wa nchi wanachama.

Wengi wanasubiri kuona ikiwa baada ya kikao cha Kamati ya Amani na Usalama kitafanikiwa kuishawishi serikali ya Burundi kupokea kikosi cha walinda amani kutoka kwa AU.

Haki miliki ya picha PSCU Kenya
Image caption Marais Uhuru Kenyatta (Kenya), Paul Kagame (Rwanda) na Macky Sall (Senegal) ni miongoni mwa waliowasili

Mwaka jana mwezi Desemba, muungano huo ulipendekeza kupelekwa kikosi cha wanajeshi 5,000 nchini Burundi kwa ajili ya kulinda amani.

Lakini Serikali ya Burundi ilipinga mpango huo na kusema kutumwa kokote kwa wanajeshi nchini mwake, kutachukuliwa kama uvamazi.

Kiongozi wa Burundi Pierre Nkurunziza alitishia kuagiza majeshi yake yashambulie wanajeshi hao wakitua nchini mwake.

Mwandishi wa BBC Sammy Awami anasema ulinzi mkali umewekwa nje na ndani ya majengo ya AU ambako mkutano huo unafanyika.