Watu watatu wauawa msikitini Saudi Arabia

Watu watatu wameuawa baada ya mtu mwenye silaha kufyatulia watu risasi katika msikiti mmoja wa Washia wakati wa sala ya Ijumaa nchini Saudi Arabia, maafisa wa serikali ya Saudia wamesema.

Watu wengine kadha wamejeruhiwa kwenye shambulio hilo katika msikiti wa Imam Reza, katika mji wa Mehasin, mashariki mwa nchi hiyo.

Mmoja wa walioshuhudia amesema waumini walimzuia mshambuliaji huyo kulipua bomu la kujitoa mhanga ambalo alikuwa amejifunga.

Maafisa wa usalama walizingira msikiti huo upesi.

Washia nchini Saudi Arabia awali wamelendwa na wapiganaji wa kundi linalojiita Islamic State.

Shambulio la leo limetokea wakati ambapo uhusiano kati ya Saudi Arabia, inayoongozwa na Wasunni, na Iran, inayoongozwa na Washia, umedorora baada ya maafisa wa Saudi kumuua mhubiri wa Kishia mwezi Desemba.