Waliokwama siku 36 mgodini Uchina waokolewa

China Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wachimba mgodi 13 bado hawajulikani waliko

Wachimbaji mgodi wanne waliokuwa wamefukiwa chini ya ardhi kwa siku 36 wameokolewa, vyombo vya habari vya serikali nchini humo vinasema.

Wanaume hao walikwama kwenye mgodi baada ya kutokea maporomoko katika machimbo ya madini ya gypsum katika mkoa wa Shandong mashariki mwa Uchina tarehe 25 Desemba.

Shirika la habari la CCTV lilionyesha picha za mmoja wa wanaume hao akitolewa chini ya ardhi na kisha kupelekwa hospitalini.

Kwa jumla, wachimbaji madini 29 walikwama baada ya maporomoko: 15 kufikia sasa wameokolewa wakiwa hai na mmoja kuthibitishwa kufariki.

Wengine 13 bado hawajulikani waliko.

Wachimbaji madini hao wane waligunduliwa wakiwa mita 200 chini ya ardhi na operesheni ya kuwaokoa ilikamilika Ijumaa.

Walifunikwa macho yao kwa barakoa walipokuwa wakitokea chini ya ardhi kuwakinga dhidi ya miali ya jua.

Vyombo vya habari vinasema wanaendelea kupimwa na kutibiwa katika hospitali moja.

Watu 400 walishiriki operesheni ya kuwaokoa.

Haki miliki ya picha CCTV NEWS

Kwa wiki kadha, wamekuwa wakichimba chini ya ardhi kujaribu kuwafikia, huku maji na vyakula vingine majimaji vikipitishwa kupitia shimo ndogo.

Ijumaa, waliokolewa mmoja baada ya mwingine, kwa kutumia kapsuli maalum.

Wachimba migodi waliokaa muda mrefu zaidi chini ya ardhi:

  • Siku 69 – Wachile 32 na raia mmoja wa Bolivia baada ya mgodi kuporomoka eneo la San Jose, Chile mwaka 2010.
  • Siku 41- Watanzania watano baada ya mgodi kuporomoka eneo la SHinganya, Tanzania 2015
  • Siku 36 – Wachimba migodi wanne wa timbo la madini ya gypsum mkoa wa Shandong, Uchina
  • Siku 14 - Raia wawili wa Australia eneo la Beaconsfield, Tasmania, mwaka 2006