Marais wapinga kutuma jeshi la AU Burundi

Haki miliki ya picha AP
Image caption AU sasa yasema haitatuma majeshi Burundi

Muungano wa Afrika AU hautatuma kikosi cha walinda amani hadi pale serikali ya rais Pierre Nkurunziza itakapotoa mwaliko.

Msemaji wa Muungano wa Afrika AU, amesema kuwa umoja huo hautatuma majeshi ya kulinda amani nchini humo hadi pale watakapopokea mwaliko kutoka kwa taifa hilo la kanda ya Afrika Mashariki.

Kauli hiyo ni kinyume na pendekezo la awali la umoja huo ambao uliibua taharuki kuhusu uhalali wake na wajibu wake wa kulinda maisha ya wananchi.

Mjumbe maalum wa umoja huo kanda ya maziwa makuu Ibrahima Fall, anasema kuwa haijawahi kuwa nia ya AU kutuma walinda amani, bila ya idhini ya taifa husika.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Nkurunziza alionya kuwa majeshi yake yangewakabili vikali jeshi hilo ''Vamizi'' akisema kuwa nchi hiyo iko salama

Mkutano wa viongozi na marais wa Afrika huko Ethiopia ulishindwa kupitisha mswada uliohitajika ilikuwatuma wanajeshi wapatao 5000 kulinda amani nchini Burundi kufuatia mauaji ya mamia ya wapinzani wa rais Nkurunziza.

Machafuko nchini humo yalitibuka baada ya Nkurunziza kutangaza nia ya kuwania uchaguzi katika muhula wake wa tatu.

Wapinzani wake walisema Nkurunziza alikuwa anakiuka katiba ya taifa na kisha maandamano yakaanza kukotokea hata jaribio la mapinduzi ambayo ilizimwa na kisha rais huyo akaibuka mshindi katika uchaguzi ambao ulisusiwa na baadhi ya viongozi wa kisiasa wa upinzani.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Machafuko nchini humo yalitibuka baada ya Nkurunziza kutangaza nia ya kuwania uchaguzi katika muhula wake wa tatu.

Kulikuwa na pendekezo la kutuma kikosi cha wapiganaji 5,000 wa muungano wa Afrika ilikuokoa maisha ya wapinzani wa rais huyo.

Awali rais Nkurunziza alionya kuwa majeshi yake yangewakabili vikali jeshi hilo ''Vamizi'' akisema kuwa nchi hiyo iko salama na kuwa ni vitongoji vichache tu vya Bujumbura ambavyo ni ngome ya upinzanani.

Kauli ya mwaka jana wa Nkurunziza kuamua kuwania urais kwa muhula wa tatu ilisababisha vurugu nchini humo, ambapo mamia ya watu wameuwawa na wengine wengi wakitorokea mataifa jirani.