Ban Ki-moon awashauri wajumbe wa Syria

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Banki Moon awaasa wajumbe wa Syria

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa, Ban Ki-moon, ametoa wito kwa wadau wote katika mzozo wa Syria kuweka tofauti zao kando kwa manufaa ya watu wa nchi hiyo na kuupa fursa mazungumzo ya amani huko Geneva.

Ujumbe wa muungano mkuu wa vyama vya upinzani wa Syria unajiandaa kukutana na mjumbe maalum wa umoja wa mataifa huko mjini Geneva leo, ambapo utaweka bayana masharti katika mazungumzo hayo.

Wajumbe wa muungano wa vyama vikuu vya upinzani nchini Syria, waliwasili mjini Geneva Switzerland kwa mkutano wa mazungumzo ya amani, yanayofadhiliwa na Umoja wa mataifa, lakini wamesizitiza kuwa wataanza mashauriano, ikiwa tu mauaji ya raia nchini humo yatasitishwa.

Msemaji wa muungano huo unaojiita kamati kuu ya mashauriano, amesema kwamba watoto wanakufa kwa njaa huku wakiwa wamezingirwa na majeshi ya serikali na baadhi yao wakiuawa na mashambulizi ya angani yanayotekelezwa na Urusi.

Anasema kuwa upinzani umefika mjini Geneva, ili kukomesha matendo hayo -- ndipo sasa mashauriano yaanze.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wajumbe wa muungano wa vyama vikuu vya upinzani nchini Syria, waliwasili mjini Geneva Switzerland kwa mkutano wa mazungumzo ya amani

Kundi hilo kuu la HNC, linasema kuwa litazungumza tu maafisa wa Umoja wa mataifa, na wala sio moja kwa moja na serikali ya Rais Bashar Al Assad.

Msemaji wa wapinzani hao anasema kuwa wanataka mashauriano hayo yafaulu.

Hadi kufikia sasa, wapinzani wamekataa katu kujadiliana na serikali ya Rais Bashar Al- Asaad Moja kwa moja, hadi pale serikali itakapokomesha mauwaji dhidi ya raia.

Mkutano huo wa mashauriano unaofadhjiliwa na Umoja wa mataifa ulianza siku ya Ijumaa, pale ujumbe maalum ulipokutana na waakilishi wa serikali ya Rais Assad.