Wakenya wahimizwa kurejea shule za zamani

Shule
Image caption Shirika hilo linasema shule zinaweza kufaidi sana kutoka kwa wanafunzi wa zamani

Shirika moja lisilo la Kiserikali limezindua kampeni ya kuwahamasisha watu waliomaliza shule kusaidia katika ukuaji na ustawi wa shule hizo.

Shirika hilo kwa jina Future First Global linawataka wanafunzi wa zamani kusaidia shule walizosomea kwa rasilimali, mafunzo na usaidizi kwa wanafunzi ambao wangali shuleni.

Bi Pauline Wanja, mmoja wa wanaoshiriki kwenye kampeni hiyo anasema lengo la mradi huo ni kusaidia shule kujikuza.

Unaendeshwa katika nchi mbalimbali, ikiwemo Uingereza, Singapore, Pakistan Cameroon na Nigeria.

“Miaka mitatu iliyopita, tuliwauliza Wakenya iwapo wanaweza kurudi kusaidia shule zao za zamani. Asilimia 78 walisema wanaweza lakini ni asilimia moja pekee walikuwa wanarudi. Wengine walisema hakuna mtu aliyewaomba kusaidia,” anasema.

Wiki yote tunawauliza warudi shuleni. Wanafunzi wa kidato cha kwanza pia wanajiunga na shule na tunawaomba kuwasaidia kwa ushauri.

Shirika hilo linabeba mabango ambayo wananchi wanaombwa kuandika ushauri ambao wangetoa kwa mwanafunzi ambaye ana umri wa miaka 16.

Mbunge wa eneo la Kibra, Nairobi Bw Ken Okoth ni mmoja wa waliorudi katika shule zao za zamani, shule ya Olympic.

“Leo tunasema asante kwa walimu, wengi bado hawajastaafu. Tunawahimiza wanafunzi wa zamani kurejea na kusaidia kwa vitabu au hata pesa,” ameambia BBC.

Kwenye mitandao ya kijamii, shirika hilo limekuwa likitumia kitambulisha mada, #asanteshule kuwahamasisha wananchi, kutoa shukran kwa shule walizosomea kwa kusaidia.