Watu 20 wauawa kwa mlipuko Afghanistan

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Vikosi vya usalama vikiwa katika eneo shambulio lilipotekelezwa mjini Kabul

Watu 20 wameuawa baada ya mtu mmoja kujitoa muhanga katika eneo la makao makuu ya Polisi mjini Kabul nchini Afghanistan, maafisa wameeleza.

Watu takriban 29 wamejeruhiwa kwenye mlipuko huo magharibi mwa Kabul,wizara ya mambo ya ndani nchini humo imeeleza.

Taarifa zinasema waliouawa na kujeruhiwa ni maafisa polisi, awali taarifa zilisema kuwa waliouawa wengi wao ni raia.

Wanamgambo wa Taliban wamekiri kuhusika na shambulio hilo, moja kati ya mashambulizi yaliyofanyika mjini Kabul na kwingineko katika kipindi cha miezi ya karibuni.

Shambulio la siku ya Jumatatu lilitokea katika lango la kuingilia jengo la makao makuu ya Polisi ambao wana jukumu la kupambana na wanamgambo wa Taliban.

Awali maafisa walisema kuwa mtu aliyetekeleza shambulio hilo aliungana na watu waliokuwa kwenye mstari kuingia kwenye kituo cha Polisi na kisha kujilipua.