Mwanamke aliyemuua mumewe asamehewa Ufaransa

Jacqueline Haki miliki ya picha EPA
Image caption Jacqueline alimuua mumewe Septemba 2010

Rais wa Ufaransa Francois Hollande amemsamehe mwanamke aliyekuwa amefungwa jela miaka 10 kwa makosa ya kumuua mumewe.

Mume wa Jacqueline Sauvage alikuwa mlevi aliyezoea kumpiga na alikuwa amembaka yeye na mabinti zake kwa miaka mingi.

Jacqueline alisema mumewe huyo pia alimnyanyasa mwana wao wa kiume, ambaye baadaye alijiua.

Watu zaidi ya 400,000 walikuwa wametia saini ombi la kumtaka Bw Hollande amwachilie huru.

Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 68 ataondoka gerezaji katikati mwa mwezi Aprili, mawakili wake wamesema.

Siku ya tarehe 10 Septemba 2010, siku ambayo mwanawe alijiua, Sauvage alimpiga risasi mumewe mara tatu akitumia bunduki.

Alipatikana na hatia na kufungwa jela miaka 10 gerezani Oktoba 2014, na kifungo chake kikadumishwa Desemba 2015 baada ya rufaa yake ya kujitetea akisema kwamba alikuwa anajikinga kukataliwa.

Kesi hiyo iliangaziwa sana Ufaransa, wengi wakitaka haki ya kutumia sababu ya kujikinga kujitetea ipanuliwe.

Walitaka watu walionyanyaswa na kudhulumiwa nyumbani waruhusiwe kutumia haki hiyo kujitetea.

Bw Hollande amefanya uamuzi wake siku mbili baada ya kukutana na mabinti watatu wa Sauvage.