Mpishi bora zaidi duniani ameaga dunia

Haki miliki ya picha AP
Image caption Mpishi bora zaidi duniani ameaga dunia

Mpishi nambari moja duniani Benoit Violier, ambaye mgahawa wake ulituzwa kwa kuwa bora zaidi duniani mwezi Desemba ameaga dunia.

Violier, 44, ni mmiliki wa mgahawa maarufu Restaurant de l'Hotel de Ville ulioko Crissier,mjini Lausanne Uswisi.

Mgahawa wake ulituzwa kwa nyota tatu za ubora wa mapishi na maandalizi ya Michelin na kuorodheshwa bora zaidi kati ya zengine 1000 na jarida la ubora wa vyakula la Ufaransa La Liste .

Polisi nchini Uswisi wanashuku mpishi huyo mzaliwa wa Ufaransa alijipiga risasi mwenyewe.

Mtandao wa habari wa 24 Heures ulisema kuwa bwana Violier alitarajiwa kuhudhuria hafla ya uzinduzi wa mbinu mpya ya kuandaa vyakula kwa hisani ya Michelin mjini Paris leo.

Kifo chake kinafwata kwa karibu kile cha mdhamini na mshauri wake Philippe Rochat, aliyemtangulia katika mgahawa wa Restaurant de l'Hotel de Ville.

Violier aliyekuwa amehudumu katika mgahawa huo kuanzia mwaka wa 1996 aliirithi pamoja na mkewe Brigitte mwaka wa 2012, kabla ya kupewa uraia wa Uswisi.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Aliwahi kuandika kitabu kikubwa kilichoelezea mbinu bora za uwindaji mbali na mapishi tofauti ya wanyama wa mwituni.

Vilevile alikuwa mwindaji shupavu.

Aliwahi kuandika kitabu kikubwa kilichoelezea mbinu bora za uwindaji mbali na mapishi tofauti ya wanyama wa mwituni.

Alituzwa na waziri wa maswala ya kigeni wa Ufaransa tuzo mbadala ya ile ya migahawa bora 50 duniani.

Wenzake wamemsifu kwa ukarimu na unyenyekevu wake.