WHO yakutana kujadili virusi vya Zika

Zika Haki miliki ya picha AFP
Image caption Virusi vya Zika vinadaiwa kufanya watoto wazaliwe na vichwa vidogo

Shirika la Afya Duniani (WHO) leo linafanya mkutano wa dharura kujadili kuenea kwa virusi vya Zika.

Mkutano huo mjini Geneva utajadili iwapo mlipuko wa virusi hivyo unafaa kutangazwa kuwa “dharura ya kimataifa”.

Maafisa wa WHO wamesema mlipuko huo wa Zika unabadilika utoka “hatari ndogo hadi kuwa wa hatari kubwa”.

Katika visa vingi, watu walioambukizwa virusi hivyo vya Zika huwa hawaonyeshi dalili zozote, lakini virusi hivyo vinadaiwa kusababisha maelfu ya watoto kuzaliwa wakiwa na vichwa vidogo Amerika Kusini.

Kutangazwa kwa mlipuko wa sasa wa Zika kuwa “dharura ya kimataifa ya afya ya umma” kutavifanya virusi hivyo kutambuliwa kama hatari kubwa duniani na kupelekea pesa, rasilimali na wataalamu wa kisayansi kutengwa kuangazia tatizo hilo Amerika Kusini na katika maabara kote duniani.

WHO inaangazia sana hasa baada ya kukosolewa kutokana na ilivyoshughulikia mlipuko wa maradhi ya Ebola Afrika Magharibi.

Wengi walisema ilichelewa sana katika kuchukua hatua, na huenda hilo lilichangia vifo vingi.

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Virusi hivyo vinaenezwa na mbu aina ya Aedes aegypti

Katika mkutano huo wa leo, wataalamu wa kudhibiti magonjwa, wataalamu kuhusu virusi na wale wanaoangazia kutengenezwa kwa chanjo, watamfahamisha mkugugenzi mkuu wa WHO Dkt Margaret Chan habari muhimu kuhusu mlipuko wa Zika.

Wiki iliyopita, alisema: “ Kiwango cha wasiwasi ni cha hali ya juu, na pia hali ya suitafahamu.

“Kuna maswali mengi, na tunahitaji majibu upesi.”