Kisa nadra cha Zika charipotiwa Marekani

Zika Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Mgonjwa aliyeambukizwa hakuwa amesafiri nje ya Marekani

Kisa nadra sana cha virusi vya Zika kuambukizwa kupitia kushiriki ngono, badala ya kuumwa na mbu, kimeripotiwa nchini Marekani.

Mgonjwa aliyeambukizwa virusi hivyo Dallas, Texas, sana huenda aliambukizwa kupitia kufanya mapenzi, Kituo cha Udhibiti wa Maradhi (CDC) kimeambia BBC.

Mtu huyo hakuwa amesafiri maeneo ambayo yana virusi hivyo lakini mpenzi wake alirejea majuzi kutoka Venezuela.

Virusi vya Zika vinaenezwa sana na mbu na vimehusishwa na visa vya watoto kuzaliwa wakiwa na vichwa vidogo na ubongo kudumaa.

Vinaenea kwa kazi Amerika na Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza hali ya tahadhari duniani.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Virusi vya Zika vinaaminika kuwafanya watoto wazaliwe na vichwa vidogo

Shirika la msalaba mwekundu nchini Marekani limewahimisha watu waliotoka maeneo yaliyoathirika na Zika, na ambao wanataka kutoa damu, wasubiri angalau siku 28, kabla ya kutoa damu.

Ushauri huu umeelekezwa kwa watu waliorejea Marekani kutoka Mexico, visiwa vya Caribbean au Amerika ya Kati na Kusini katika kipindi cha wiki nne zilizopita, shirika hilo limesema kupitia taarifa.

Katika tukio jingine, visa viwili vya maambukizi ya Zika vimethibitishwa Australia.

Maafisa wanasema wakazi wawili wa Sydey waliopatikana na virusi hivyo walirejea kutoka Caribbean majuzi.

Kisa hicho cha maambukizi ya Zika Dllas, kitakuwa ndicho cha kwanza kuthibitishwa kutokea Marekani bara, ingawa jimbo la Texas limeripoti visa vingine ssaba, vyote kwenye watu waliorejea kutoka nje.

Anne Schuchat, naibu mkurugenzi mkuu wa CDC amesema hicho ndicho kisa cha kwanza kinachohusisha mtu ambaye hakusafiri.

"Hatudhani aliambukizwa baada ya kuumwa na mbu, lakini tunaamini aliambukizwa kupitia kushiriki ngono.”

Taarifa ya CDC imesema njia bora zaidi ya kujikinga na “kujikinga usiumwe na mbu na kutokumbana na manii kutoka kwa mtu aliyekumbana na virusi vya Zika”.

Kisa hicho hata hivyo sicho cha kwanza kabisa cha maambukizi kupitia ngono kuripotiwa.

Shirika la CDC linasema kwenye tovuti yake kwamba mwaka 2013 kulilipotiwa kisa cha maambukizi kupitia kushiriki mapenzi katika jimbo la French Polynesia.

Shirika hilo linawashauri wanawake wajawazito kutosafiri mataifa mengi yaliyoathiriwa sana na virusi hivyo.