Kesi ya Bill Cosby kuhusu unyanyasaji kuendelea

Haki miliki ya picha AP
Image caption Bill Cosby

Waendesha mashtaka nchini Marekani wanaweza kuendelea na mashtaka ya unyanyasaji wa kingono dhidi ya msanii wa ucheshi Bill Cosby,jaji mmoja ameamuru.

Bwana Cosby anatuhumiwa kwa kumlewesha na kumpapasa mfanyikazi wa chuo kikuu cha Temple mwaka 2004.

Siku ya jumatano,Jaji mmoja katika jimbo la Pennsylvania alikataa hoja iliowasilishwa na mawakili wake kwamba uamuzi wa hapo awali mwaka 2005 ulimpatia kinga ya kutoshtakiwa.

Makumi ya wanawake wamesema kuwa nyota huyo aliwanyanyasa lakini nyota huyo wa zamani wa runinga anasema kuwa mikutano hiyo ilikuwa na idhini kutoka pande zote mbili.

Awamu inayofuata ya kesi hiyo ni uamuzi wa iwapo kuna ushahidi wa kutosha kwa Cosby kushtakiwa.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Bill Cosby

Mcheshi huyo ,ambaye aliwahi kuwa nyota anayelipwa fedha nyingi wakati mmoja ,huenda akahukumiwa kifungo cha miaka 10 jela iwapo atapatikana na hatia.

Jaji Steven O'Neil alitoa uamuzi huo katika mahakama moja huko Norristown,nje ya jimbo la Philadelphia baada ya kusikiza kesi hiyo kwa siku mbili.

Malalamishi ya Andrea Constand,ambaye hakutaka kujulikana yaliwasilishwa kwa mara ya kwanza baada ya madai hayo ya unyanyasaji.

Lakini aliyekuwa wakili wa wilaya,Bruce Castor,aliamua kwamba hakuna ushahidi wa kutosha kuanzisha mashtaka.

Hatahivyo mawakili waliomrithi bwana Castor mwaka uliopita waliamua mwaka uliopita kuifungua upya kesi hiyo baada ya wanawake wengine kujitokeza na madai kama hayo.