Clinton na Sanders wakabiliana kwenye mdahalo

Sanders Clinton Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Sanders na Clinton ndio wagombea pekee waliosalia chama cha Democratic

Hillary Clinton na Bernie Sanders wamekabiliana kuhusu kudhibitiwa na matajiri wa Wall Street pamoja na sera ya mashauri ya kigeni, kwenye mdahalo wa kwanza wa chama cha Democratic msimu huu kushirikisha wagombea wawili pekee.

Bi Clinton amemweleza Bw Sanders kama mtu mdhanifu ambaye hataweza kutekeleza mambo mengi anayopgania.

Bw Sanders naye amesema Bi Clinton ni mtu ambaye amejikita sana katika mfumo wa sasa wa utawala na hawezi kutekeleza mageuzi.

Mdahalo huo wa runingani katika jimbo la New Hampshire ulikuwa wao wa kwanza tangu kusalie na wagombea wawili pekee chama cha Democratic wiki hii.

Bila kuwepo na mtu wa tatu jukwaani, tofauti za kisera kati ya wawili hao zimeanikwa wazi.

Waziri huyo wa zamani wa mashauri ya kigeni amesema mapendekezo ya Bernie Sanders kama vile huduma ya afya kwa wote ni ghali mno na hayawezi kutimizika.

Na pia amejibu vikali jaribio la mpinzani wake la kutaka kumuonesha kama mtu anayedhibitiwa na matajiri wa Wall Street kwa sababu pesa nyingi zake za kampeni zimetoka kwa wahisani pamoja na ada za kutozwa baada ya kutoa hotuba kwenye dhifa za jioni.

"Wakati umefika wewe na watu wako wa kampeni mkomeshe kampeni hii ya kunipaka matope,” amesema.

Bw Sanders, seneta wa Vermont, alitumia tena Vita vya Iraq kumshambulia Bi Clinton akisema aliunga mkono vita hivyo.

Hata hivyo, Bi Clinton naye ametilia shaka ujuzi wa Sanders katika masuala ya sera za mashauri ya kigeni.

Image caption Clinton alipata ushindi mwembamba mchujo wa Iowa

Mdahalo huo umetokea siku tano kabla ya mchujo wa pili wa vyama kuteua wagombea kufanyika New Hampshire tarehe 9 Februari.

Licha ya kupingana vikali kuhusu sera, wawili hao walikamilisha mjadala kwa urafiki kiasi, Clinton akisema kwamba mtu wa kwanza ambaye atampigia simu iwapo atashinda uteuzi ni Bw Sanders.

Mdahalo huo ulikuwa wa kwanza bila gavana wa Maryland Maryland, Martin O'Malley, aliyejiondoa baada ya kutofana mchujo wa Iowa.

Bi Clinton alipata ushindi mwembamba dhidi ya Bw Sanders, huku Bw O’Malley akimaliza nyuma sana.

Bw Sanders anaongoza New Hampshire kwenye kura za maoni. Jimbo hilo linapakana na jimbo la Vermont.

Uchaguzi mkuu nchini Marekani utafanyika Novemba.