Dhahabu ya $18,000 yakosa mwenyewe Ujerumani

Haki miliki ya picha Bavaria Police

Msichana mmoja nchini Ujerumani ameruhusiwa kumiliki kipande cha dhahabu cha thamani ya €16,000 ($18,000; £11,500) ambacho alikipata katika ziwa moja.

Polisi wanasema ameruhusiwa kukaa nacho baada ya mmiliki wake kukosekana.

Msichana huyo wa umri wa miaka 16 alipata kipande hicho cha dhahabu cha gramu 500 mita 2 chini ya maji alipokuwa akiogelea katika ziwa la Koenigssee, jimbo la Bavaria, Agosti mwaka jana.

Alikisalimisha kwa polisi ambao hadi sasa hawajampata mwenyewe.

Haijabainika ni vipi kipande hicho kilifika huko.

Uchunguzi wa miezi sita haukufanikiwa kufichua mmiliki halisi.

Kupatikana kwa dhahabu hiyo kumefufua uvumi wa kuwepo kwa dhahabu iliyomilikiwa na watawala wa Nazi ambayo ilidaiwa kupotea karibu na ziwa hilo lililoko karibu na mpaka wa kusini wa Ujerumani na Austria.