Mwanamuziki nyota Maurice White afariki dunia

White Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Maurice White aligunduliwa kuwa na ugonjwa wa kutetemeka 1992

Mwanamuziki nyota wa nyimbo za mtindo wa Soul Maurice White, aliyeanzisha kundi maarufu la wanamuziki la Earth, Wind and Fire miaka ya sitini amefariki dunia.

Alijulikana kwa vibao kama vile September, Boogie Wonderland, Shining Star na After the Love has Gone.

Amefariki akiwa na umri wa miaka 74 akiwa usingizini Los Angeles, kakake Verdine White amesema.

Kundi hilo lilimshirikisha kakake na pia mwanamuziki Philip Bailey.

Wanamuziki hao kwa pamoja walichomoa vibao vilivyovuma sana miaka ya sabini.

Haki miliki ya picha AP
Image caption White ndiye mwanzilishi wa bendi ya Earth Whind and Fire

Kwa jumla, waliuza zaidi ya albamu milioni 90 kote duniani na kushinda tuzo sita za Grammy.

Maurice White, aliyejulikana sana kama Reese, alijiondoa Earth Wind And Fire mwaka 1995.

Alifichua hadharani kwamba alikuwa akiugua ugonjwa wa kutetemeka (Parkinson) miaka mitano baadaye wakati bendi hiyo ilipokuwa ikiingizwa rasmi kwenye Rock and Roll Hall of Fame.

White pia alifanya kazi kama produsa, akifanya kazi na wanamuziki wengine maarufu kama vile Barbra Streisand, Cher na Neil Diamond.