UN: Walinda amani CAR wamefeli

walinda amani wa CAR
Image caption Walinda amani wa CAR

Umoja wa Mataifa umekiri kwamba wanajeshi wake wa kulinda amani katika Jamuhuri ya Afrika ya Kati walistahili kuimarisha utendakazi wake.

Hii ni baada ya ripoti ya shirika la kutetea haki za binadamu Amnesty International kusema wanajeshi hao hawatekelezi majukumu yao ipasavyo.

Mkuu wa kikosi hicho Parfait Onanga-Anyanga amesema kikosi hicho hakikutarajia kuzuka kwa ghasia katika mji mkuu Bangui hapo mwezi Septemba mwaka uliopita.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Raia wengi wamekimbia makaazi yao kutokana na vita CAR

Machafuko hayo yalisababisha vifo vya zaidi ya watu 70. Wanajeshi hao waliweza kuzima ghasia hizo na kuweka mikakati mipya kuzima ghasia katika siku zijazo.

Bwana Onanga amesema wanajeshi wake walifanikiwa kusimamia ziara ya Papa hapo mwezi Novemba sawa na uchaguzi mkuu uliofanyika mwezi Decemba mwaka uliopita.

Jamuhuri ya Afrika ya Kati ilitumbukia kwenye vita vya kidini baada ya waasi waisilamu wa kundi la Seleka kupindua serikali mwaka wa 2013, na hivyo kuchochea machafuko ya kulipiza kisasi kutoka kwa wapiganaji Wakristo wa kundi la Anti-balaka.