Wakili amshtaki mungu wa Kihindi India

Ram
Image caption Ram ni mmoja wa miungu wanaoabudiwa na kutukuzwa sana na Wahindi

Wakili mmoja nchini India ameshangaza wengi baada ya kuwasilisha kesi dhidi ya mungu anayetukuzwa sana na Wahindi kwa jina Ram.

Wakili huyo Chandan Kumar Singh anasema “Bwana Ram alimdhalilisha mkewe Sita".

Alitaka mahakama katika jimbo la Bihar, mashariki mwa India, ithibitishe hilo.

Ram ndiye huangaziwa kwenye Ramayana, utenzi wa beti 24,000 ulioandikwa kwa lugha ya Kisanskrit.

Huabudiwa na mamilioni ya watu India na kote duniani.

Bw Singh anaamini kwamba kesi yake ina msingi.

Ananukuu vitabu vya kidini kutetea hilo.

“Inajulikana wazi kwamba Ram alimtaka Sita athibitishe kwamba bado alikuwa msafi baada yake kumuokoa kutoka kwenye minyororo ya mfalme muovu Ravana. Hakumuamini Sita," Bw Singh ameambia BBC.

Haki miliki ya picha Hemendra Kumar Singh
Image caption Wakili Chandan Kumar Singh anasema anataka wanawake waheshimiwe

Kesi yake ya kwanza ilitupwa na mahakama wiki iliyopita lakini anasema atawasilisha kesi nyingine.

"Jinsi Ram alivyomchukulia Sita ni dhihirisho kwamba wanawake hawakuheshimiwa hata zamani. Ninajua hili huenda likaonekana suala la kipumbavu, lakini lazima tujadili tamaduni zetu za kidini. Nitawasilisha kesi upya kwa sababu ninaamini kwamba Wahindi sharti wakubali kwamba Ram alimdhalilisha Sita."

Bw Singh amepuuzilia mbali madai kwamba anajitafutia tu sifa.

Amesema watu hawawezi kuendelea kujadili kuhusu kuheshimiwa kwa wanawake ilhali inajulikana wazi kwamba miungu huyo anayeabudiwa na wengi hakumheshimu mkewe.

Hatua yake imeshutumiwa vikali hata na wenzake.

Baadhi wametishia kumshtaki na wengine kuomba chama cha wanasheria nchini humo kumpokonya leseni ya uanasheria.

“Huwa twawatazama Ram na Sita kwa pamoja na huwaabudu walivyo kwa pamoja. Hakuna suala la kuamini kwamba Ram alimdhalilisha Sita,” Ranjan Kumar Singh, mmoja wa wanaompinga anasema.