Wimbi la uchezaji kamari lavuma Kenya

Mashabiki
Image caption Wengi wanatumia simu kuweka dau

Katika mikusanyiko ya watu nchini Kenya siku hizi, ni kawaida kuwasikia watu wakisimulia walivyojishindia pesa kwenye mashindano ya bahati nasibu.

Wimbi hili limewateka wengi, wakubwa kwa wadogo, wazee kwa vijana.

Zamani watu walikuwa wakishiriki kwa kununua kadi, kutembelea kasino au kucheza kwenye ‘pata potea’ katika barabara za mitaa lakini siku hizi mambo yamebadilika.

Wengi wanashiriki kwa kutumia simu au kutembelea tovuti mtandaoni

Yanayovuma kwa sasa ni mashindano yanayohusu michezo ambapo washiriki wanabashiri matokeo na kuahidiwa kushinda mamilioni ya pesa.

Mwandishi wa BBC Emmanuel Igunza alijitosa mitaani Nairobi kuchunguza zaidi kuhusu wimbi hili la bahati nasibu.

Katika mtaa mmoja alikutana na kundi la vijana wakijadili shindano moja, huku kila mmoja akitumai kwamba karibuni ataangukiwa na bahati na kujishindia mamilioni.

Image caption Vijana wengi wanashiriki katika mashindano hayo ya kubashiri matokeo ya mechi

Wanachohitaji ni simu ya kawaida tu na takriban dola moja hivi ya Marekani kabla ya kuanza kushiriki michezo hiyo.

Wanaweza kuweka dau kuhusu matokeo ya mechi za soka za ligi nyingi duniani, kuanzia ligi zinazovuma Ulaya hadi kwa zile zisizojulikana sana Asia na Mashariki ya Kati.

Hutakosa watu wakizungumza kuhusu SportPesa, Betin, Betway, Oxygen 8, Justbet au mCHEZA, kampuni zinazotumia simu kuendesha michezo ya bahati nasibu.

Mmoja wao ni Fanuel Kadenge, ambaye amefanya kazi kama fundi wa viatu kwa miaka mitano.

Mapato yake ni takriban $10 kwa siku. Shabiki huyo sugu wa klabu ya Arsenal hucheza shindano la bahati nasibu angalao mara tano kwa wiki, hata anapopungukiwa na pesa.

“Nitaendelea kucheza. Hakuna anayeweza kukunyima kitu iwapo Mungu ameamua kwamba utapata,” anasema Bw Kadenge.

Huwezi kusikiliza tena

Inakadiriwa kwamba biashara ya mashindano ya bahati nasibu itakuwa na thamani ya $50 milioni nchini Kenya katika kipindi cha miaka mitatu ijayo.

Kwa mujibu wa ripoti ya shirika la ukaguzi wa hesabu la PricewaterhouseCoopers, mwaka 2014 mapato yaliyotokana na mashindano ya bahati nasibu Kenya yalifikia $20 milioni, likiwa ongezeko la 6% kutoka mwaka uliotangulia.

Mwishoni mwa wiki, moja ya kampuni zinazoandaa mashindano hayo iliandaa hafla kubwa jijini Nairobi ambapo waliohudhuria walitumbuizwa na wasanii nyota kutoka Kenya.

Kila saa, kulikuwa kukitangazwa washindi wa $500.

Hivi majuzi, mwanamke mmoja kutoka magharibi mwa Kenya alijishindia $220,000 baada ya kubashiri kwa ufasaha matokeo ya mechi 13 za ligi za Uingereza, Uhispania na Italia.

Ni ushindi kama huo ambao wengi wa wanaoshiriki wanatafuta.

Lakini si wote wanaobahatika, na mwanasaikolojia Sammy Wambugu anasema wengi wanaishia kutumbukia kwenye uraibu huo bila kujua watajinasua vipi.

Anasema tatizo ni kwamba anayeshiriki huamini kwamba kila wakati anakaribia sana kushinda.

"Lakini si hivyo. Unaweza ukacheza maisha yako yote bila kushinda."